Alhamisi 27 Agosti 2026 - 18:52
Umoja wa Waislamu; Msingi Uliojikita katika Muundo wa Maarifa ya Uislamu

Hawzah/ Umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu, ambao unapita zaidi ya masuala ya kikabila, rangi na hata tofauti za kimadhehebu, ni ulazima wa kidini na kiakili; kwani Uislamu mtukufu hauruhusu Waislamu kubadilika na kuwa tabaka zinavyogombana na kupingana wao kwa wao.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Imam na Kiongozi wetu Shahidi, mnamo mwaka 1400 Hijria Shamsia, wakati wa kumbukumbu yenye baraka ya kuzaliwa kwa furaha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) na Imam Jaafar Sadiq (as), katika mkutano wake na baadhi ya viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu pamoja na wageni walioshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu, alisema: “Umoja na mshikamano wa Waislamu si jambo la kimkakati la muda ambalo baadhi ya watu wanaweza kudhani kwamba, kwa sababu ya mazingira maalumu, tunapaswa sasa kuwa na umoja pamoja. La hasha, bali ni jambo la msingi.”

Umoja uliojikita katika matabaka ya kijamii

Sayyid Rasul Mousavi, mtafiti katika masuala ya kimataifa na mwanadiplomasia wa zamani, anaamini kwamba mtazamo na mwelekeo wa Kiongozi wetu Shahidi kuhusu suala la umoja wa Kiislamu ulikuwa ni mtazamo wa kimsingi na wa kimkakati.

Aidha, akifafanua suala hili, alisema: “Mtazamo wa Imam na Kiongozi Shahidi kuhusu suala la umoja wa ulimwengu wa Kiislamu tangu mwanzo ulijengwa juu ya utofauti mmoja muhimu: utofauti kati ya serikali kama wahusika rasmi katika mfumo wa kimataifa, na mataifa kama wabeba utambulisho, matakwa na nguvu ya kijamii. Katika mfumo huu wa fikra, umoja wa Kiislamu haukufafanuliwa tu kama mradi wa kidiplomasia au unaotegemea makubaliano baina ya serikali, bali ulijikita katika matabaka ya kijamii, ya wananchi na yaliyoandaliwa. Bila shaka, serikali haziondolewi katika mfumo huu wa fikra na zina nafasi yao, lakini msisitizo mkuu unawekwa kwenye uwezo unaojengwa ndani ya jamii na unaodhihirika kupitia nguvu za Muqawama na kile kinachoitwa ‘Mbele ya Muqawama.’”

Mtafiti huyo wa masuala ya kimataifa ameongeza: “Kama vile Mapinduzi ya Kiislamu ndani ya nchi yalivyotegemea wananchi, katika ngazi ya eneo pia kipengele cha wananchi kina nafasi ya kuamua; hivyo, matarajio ya mabadiliko ya msingi katika asili ya kimtazamo wa wananchi nje ya mipaka hayana msingi wa kutosha. Hii ni kwa sababu kipengele cha wananchi, hususan katika suala la umoja na mshikamano wa Umma wa Kiislamu, si sehemu ya kimkakati ya muda, bali ni sehemu ya utambulisho wa kimkakati wa mtazamo huu.”

Umoja; ulazima wa kidini na kiakili

Kwa upande mwingine, inapaswa kupewa umuhimu maalumu nukta hii ya msingi kwamba dini tukufu ya Uislamu, ikiwa ni dini kamili zaidi miongoni mwa dini za Mwenyezi Mungu, imejenga msingi wake juu ya “udugu wa kiimani.”

Katika muktadha huo, Qur’ani Tukufu inasema wazi kabisa:

“إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ”

“Hakika Waumini ni ndugu.”

Udugu huu unapita zaidi ya mipaka ya kikabila, kirangi na hata tofauti za kimadhehebu; kwani pamoja na Uislamu kukubali kuwepo kwa utofauti wa madhehebu, hautoi ruhusa kwa Umma wa Kiislamu kubadilika na kuwa tabaka zinazogombana na kupingana wao kwa wao.

Jambo jingine muhimu ni kwamba: Tofauti zilizopo kati ya Shia na Sunni, ingawa zinaweza kujadiliwa na kuchunguzwa katika uwanja wake wa kielimu, hazipaswi kuwa sababu ya kukataa utambulisho wa Kiislamu wa upande mwingine au kuwa chombo cha migogoro na fitina za kuwatenganisha Waislamu. Kwa vyovyote vile, misingi inayowaunganisha Waislamu wa madhehebu mbalimbali ni mipana zaidi kuliko maeneo ya tofauti zao. Kwa hiyo, kuacha mambo yanayowaunganisha na kushikilia masuala yenye tofauti hakutazaa matokeo mengine isipokuwa kukamilisha fumbo lililoundwa na maadui kwa lengo la kuleta mgawanyiko kws mwa Waislamu.

Kwa kweli, swali linapaswa kuulizwa: Kutukana matakatifu ya kidini ya watu wa madhehebu mengine kuna manufaa gani ambayo madhehebu fulani linaweza kuyapata? Na je, kupitia matukio ya aina hii wanaweza kumvutia mtu kwenye upande wao, au badala yake wanawafanya hata baadhi ya watu wa kundi lao wenyewe kuwachukia?

Umoja wa Waislamu; jambo lisiloweza kupingika

Kwa kuzingatia mambo yaliyotajwa, tunaweza kusema wazi kwamba hata kwa mtazamo wa kiakili, umoja ni ulazima usioweza kupingika. Inapaswa kuzingatiwa kwamba ulimwengu wa Kiislamu, ukiwa na idadi ya watu takribani bilioni mbili, ukiwa na utajiri mkubwa zaidi wa rasilimali za asili, nafasi ya kipekee ya kijiografia na kisiasa, pamoja na urithi mkubwa wa kistaarabu, iwapo utaungana unaweza kubadilika na kuwa nguvu isiyo na mfano katika mizania ya dunia.

Kinyume chake, mgawanyiko na migogoro ya ndani hupoteza uwezo huu mkubwa na kuwaweka Waislamu katika hali ya udhaifu, kutokuwa na mwitikio na utegemezi. Aidha, uzoefu mchungu wa karne kadhaa zilizopita, kuanzia ukoloni hadi uvamizi na uingiliaji wa kijeshi, yote yaliwezekana chini ya kivuli cha mgawanyiko na kutokuwepo kwa mshikamano wa ndani katika ulimwengu wa Kiislamu.

Suluhisho la Qur’ani la kuimarisha umoja wa Kiislamu

Qur’ani Tukufu, katika aya za katikati za Surat Al-Hashr, kuanzia aya ya 9 hadi ya 14, inawasilisha kwa Waumini mkakati mpana na wa kina kuhusu umoja na mshikamano wa Kiislamu, ambapo umoja unainuliwa kutoka kuwa mbinu ya muda na kuwa uhusiano wa moyo na akili.

Mola wa walimwengu, katika kuelezea jamii bora ya Waumini, kwanza anasisitiza “kujitoa kwa ajili ya wengine” na “mapenzi”, kisha anaeleza kwamba msingi wa umoja ni kuacha maslahi binafsi kwa manufaa ya ndugu katika dini.

Katika aya ya 10 ya Surat Al-Hashr, anaendeleza uhusiano huu katika mwendelezo wa historia; pale Waumini wanapomuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu ajaalie chuki yoyote dhidi ya Waumini wengine ndani ya nyoyo zao:

“وَلَا تَجْعَلْ فِی قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِینَ آمَنُوا”

“Wala usijaalie katika nyoyo zetu chuki yoyote dhidi ya walioamini.”

Hii ina maana kwamba umoja wa Kiislamu unahitaji kuisafisha nafsi kutokana na misimamo ya kibaguzi na misimamo mikali inayosababisha mgawanyiko.

Kwa upande mwingine, Qur’ani imeeleza kwamba mshikamano wa safu ya maadui ni dhana ya uongo isiyokuwa na msingi, na inasema:

“تَحْسَبُهُمْ جَمِیعًا وَقُلُوبُهُمْ شَتَّی”

“Unawadhania kuwa wameungana, ili hali nyoyo zao zimegawanyika.”

Sababu ya kutawanyika kwa nyoyo za watu wa batili pia imeelezwa kuwa ni kujitenga na mantiki na busara:

“قَوْمٌ لَّا یَعْقِلُونَ”

“Ni watu wasio na akili.”

Kwa mujibu wa aya hizi, umoja wa Kiislamu umejengwa juu ya misingi mitatu:

1. Mapenzi na kujitoa kwa ajili ya wengine katika uwanja wa vitendo;

2. Nyoyo zilizotakata kutokana na chuki dhidi ya Waumini wengine;

3. Uhusiano wa moyo unaojengwa juu ya mantiki na busara ya kidini, ambao unasimama kinyume na umoja wa kujifanya na wa kimkakati wa muda wa safu ya maadui.

Sayyid Muhammad Mahdi Mousavi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha